Nachukua fursa hii kukupeni mkono wa pole wasikilizaji wetu wapenzi na hasa wafuasi wa Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW, kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyokufa shahidi Imam Ridha (as) na kukukaribisheni kusikiliza machache niliyokuandalieni kwa mnasaba huo.
Imam Ridha (as), ambaye ni Imamu wa nane wa Waislamu wa Kishia, alishika hatamu za Uimamu na uongozi wa umma akiwa na umri wa miaka 35. Kutokana na baba yake mpenzi Imam Musa Kadhim (as) kuwekwa kizuizini katika jela za Basra na Baghdad na kukatika mawasiliano baina yake na wafuasi wake, Imam Ridha alikuwa ndiye kiunganishi baina ya Imam Kadhim (as) na watu. Zama za Uimamu wa Imam Ridha (as) zilisadifiana na tawala za makhalifa watatu wa Bani Abbas, yaani Harun, Amin na Maamun; ambapo miaka mitano ya mwisho ya Uimamu wake ilimalizikia katika ukhalifa wa Maamun, mmoja wa makhalifa wajanja zaidi na wenye hila na ghilba kubwa zaidi, miongoni mwa makhalifa wa Bani Abbas. Awali Maamun alimpendekezea Ukhalifa Imam Ridha, lakini alipolikataa pendekezo hilo, alimwambia, kama haukubali Ukhalifa, basi lazima aridhie kuwa mrithi wa khilafa baada yake.
Jibu na hatua ya kwanza aliyoichukua Imam Ridha (as) kuhusiana na kuteuliwa kwa nguvu kuwa mrithi wa ukhalifa ilikuwa ni kukataa kwenda Marw, yalikokuwako makao makuu ya utawala wa Maamun, mpaka askari wa khalifa huyo wa Bani Abbas wakamlazimisha Imam ahamie huko kwa nguvu. Lakini nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba, kuikubali nafasi ya mrithi wa ukhalifa ilikuwa fursa ambayo Imam Ridha (as) aliitumia kuiletea matunda na mafanikio jamii ya Kiislamu ya zama hizo. Mtukufu huyo alikutumia kuteuliwa kwake kuwa mrithi wa ukhalifa ili kuitambulisha kwa watu haki ya Ahlul-Bayt pamoja na kuhuisha dini sahihi aliyokuja nayo Bwana Mtume Muhammad SAW.
Ndani ya ardhi ya Iran na maeneo ya mashariki ya Ulimwengu wa Kiislamu, kilipatikana kiwango fulani cha watu ambao waliingia kwenye madhehebu ya Shia kwa njia ya moja kwa moja au kupitia wajumbe wa Imam aliyetangulia; na kulikuwa na watu wengi ambao hawakuwa na ufahamu wowote wa kumjua Imam Ali Ibn Musa Ridha (as). Kwa hivyo kwa kuteuliwa Imam kuwa mrithi wa khalifa, wapenzi wa Ahlul Bayt walipata moyo na faraja kubwa na kuweza kupumua na kupungukiwa na mbinyo na mashinikizo yaliyokuwa yakiwaandama; na kwa baraka za Imam Ridha (as), Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume SAW wakawa wanatajwa kwa heshima na wema kila mahali; na watu ambao hawakuwa wakiujua utukufu wa watu wa Nyumba ya Bwana Mtume, wakabahatika kuwaelewa kwa karibu waja hao wateule.
Lakini mbali na hayo, kuhudhuria Imam Ridha (as) vikao vya mijadala na midahalo, ambayo Maamun alikuwa akiiandaa kwa madhumuni ya kuitia doa hadhi ya kielimu ya mtukufu huyo kwa kuwaalika maulamaa wa dini na madhehebu nyenginezo, yote hayo yalizidi kudhihirisha daraja adhimu na tukufu ya kielimu ya Imam Ridha (as) na kuwafanya maulamaa wa dini mbali mbali wabainikiwe na bahari yenye kina kisicho na ukomo na ubobeaji usio na mpaka wa Imamu huyo kwa kila taaluma ya dini. Mapambano ya siri lakini yenye lengo maalumu aliyoyaendesha Imam Ridha (as) dhidi ya mihimili na mizizi ya dhulma na uonevu, yalikuwa na taathira kubwa, kiasi kwamba baada ya propaganda chafu za miaka na miaka zilizofanywa na tawala za kidhalimu dhidi ya Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume, utukufu na adhama ya kimaanawi ya Maimamu hao madhulumu ilizidi kudhihirika, na kauli zilizotanda na kuenea katika anga ya jamii zilikuwa za kuwatukuza na kuwaenzi Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume SAW hususan Imam Ridha (as). Kutokana na hali hiyo, Maamun, ambaye alishindwa kufikia malengo yake, kwa kutoweza kujinufaisha kivyovyote vile na hatua yake ya kumfanya Imam Ridha mrithi wa ukhalifa wake licha ya kujikurubisha kimaonyesho kwa mtukufu huyo, hakuchelea kumuua shahidi mjukuu huyo mtoharifu wa Mtume wa Allah kwa ajili ya kuulinda ukhalifa wake. Imam huyo mtukufu, kama walivyokuwa mababu zake watakasifu alihitari kufa shahidi katika njia ya kupambana na dhulma, lakini hakuridhia madhila ya kushirikiana na kuunga mkono utawala wa kijabari na kiimla wa Maamun. Wananchi wa Iran wanajivunia kuwa wenyeji na wapokezi wa shakhsia huyo adhimu; na kila siku huwa wanaizuru haram yake toharifu ili kupata heri na baraka zake.
Imam Ridha (as) alikuwa na nemsi za kielimu na sifa nyingi mno njema za kiakhlaqi. Mtukufu huyo ambaye alikuwa bahari isiyo na ukomo wa kina ya elimu ya dini na akapambika kwa tabia njema za babu yake Bwana Mtume Muhammad SAW, alikuwa kila mara akitilia mkazo kuchungwa haki za watu wa matabaka yote katika jamii. Suleiman Ibn Jaafar Abu Hashim Jaafari, anayejulikana kama mmoja wa wapokezi watajika na waaminifu katika madhehebu ya Imamiyyah, akiwa amebahatika kuishi katika zama za Maimamu wanne wa Kishia,ambao ni Imam Ridha, Imam Jawad, Imam Hadi na Imam Hassan A’skari (as), anasimulia kwamba, siku moja nilikuwa pamoja na Imam kwa ajili ya kushughulikia baadhi ya mambo. Nipomaliza kazi yangu na nikamwomba ruhusa ya kuondoka, Imam alinambia: “Baki na sisi kwa usiku wa leo.” Kwa hivyo nikafuatana na Imam hadi nyumbani kwake. Jua lilikuwa linakaribia kuchwa na maghulamu wa Imam walikuwa wanafanya kazi ya uashi. Imam Ridha aliona mmoja wao ni sura ngeni kwake, hivyo akauliza: Huyu ni nani? Wakamwambia: Ni kibarua anayetusaidia kazi na sisi tunamgaia chochote. Imam akawauliza: Mumemuainishia ujira wake? Wakajibu: Hapana! Chochote tunachomkadiria anapokea. Imam hakupendezwa na jambo lile, akasema: Nimeshawaambia hawa mara kadhaa, msimlete mtu yeyote kufanya kazi, mpaka mhakikishe mumemuainishia ujira wake kabla hajafanya kazi. Mtu anayefanya kazi bila mkataba na kuainishiwa ujira, hata ukimpa mara tatu ya ujira wake, atahisi tu kwamba umempa ujira mdogo; lakini kama utafunga naye mkataba, na kumlipa kiwango kilichoainishwa cha fedha atafurahika na wewe, kwamba umemfanyia kwa mujibu wa mkataba wenu; na kama utamuongeza chochote zaidi ya kile kilichoainishwa, hata kama kitakuwa kichache na haba, atafahamu kuwa umempa zaidi ya ujira wake na atashukuru.”Kujituma kwa ajili ya kuhangaikia maisha na kuikimu mtu familia yake ni moja ya sifa muhimu zaidi ya wema wanayohisabika kuwa nayo watu walio waumini wa kweli. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, kujituma mtu ili kuyumudu maisha yake ni sawa na “kupigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu”; na mtu anayekufa katika njia hiyo anahisabika kuwa amekufa “shahidi” mbele ya Allah. Na ndiyo maana jasho linalomchirizika kibarua ni sawa na damu ya shahidi, inayomwagika katika njia ya Allah, kwenye medani ya jihadi. Katika kuelezea malipo ya kibarua anayejituma, Imam Ridha (as) amesema: “Kwa hakika mtu anayeshughulika kujiongezea riziki yake ili aweze kukimu familia yake, malipo yake ni makubwa zaidi ya anayepigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Wapenzi wasikilizaji, wasia huu wa Imam wa Nane (as) ni wa kuufanyia kazi katika mazingira yoyote yale; na utekelezaji wake unahitajika kikamilifu katika zama zetu hizi. Kuchunga haki za kiutu kwa watu wote katika jamii, ni jambo muhimu zaidi la kujenga maelewano sahihi na chanya ya kijamii na kidini, katika jamii ya Kiislamu. Mwajiri anayemfanyisha kazi kibarua, anapaswa kabla ya jambo lolote lile, azingatie haki zake za kiutu; na jambo la msingi kabisa ni kumlipa ujira wake kwa usahihi na kwa ukamilifu.
Uislamu ni dini ya kulinda heshima ya mwanadamu, na ndio maana alipozungumzia sifa ya dini hiyo inayotetea uadilifu, Imam Ridha (as) alisema: “«فان الناس لو علموا محاسن کلامنا لاتّبعونا»، “Hakika lau kama watu wangejua uzuri wa maneno yetu, wangelitufuata.” Kwa hivyo ni wajibu wetu sote kulinda heshima ya vibarua na kutambua kwamba, tunapowaheshimu vibarua huwa kwa hakika tunawakirimu waja wa Mwenyezi Mungu wanaohangaika na kujituma ili kuweza kukimu maisha yao na kujipatia chumo na riziki ya halali.
Wapenzi wasikilizaji, kwa mara nyingine tena ninakupeni mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyokufa shahidi Imam Ali Ibn Musa Ridha (as); na tunahitimisha kipindi hiki maalumu kwa hadithi ya mtukufu huyo ninayoinukuu katika kitabu cha U’yunu-Akhbari-Ridha kilichoandikwa na al Marhum Sheikh Saduq. Imam Ridha (as) amesema: “Yeyote atakayenizuru licha ya umbali wa masafa, na akatoka masafa ya mbali ili kuja kunizuru, nitakuja kumsaidia katika sehemu tatu Siku ya Kiyama ili kumuokoa na fazaa ya sehemu hizo. “Kwanza ni wakati madaftari ya amali yatapogawanywa kuliani na kushotoni. Pili ni wakati wa kupita katika Sirati. Na tatu ni wakati amali zake zitakapopimwa.” Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/
342/